Tuesday, August 22, 2017

SIFA 6 ZA MWANAUME ANAYESTAHILI KUWA MUMEO!

Wiki hii nitazungumzia sifa 6 za mwanaume ambaye anastahili kuwa mumeo. Nafanya hivi ikiwa ni msaada kwa wale ambao wamefikia hatua ya kuingia kwenye ndoa lakini bado wanashindwa kutambua yupi ni sahihi na yupi si sahihi kuitwa mume.
Tufahamu kwamba si kila mwanaume unayekutana naye na ukampenda anafaa kuwa mumeo. Wengine wana mapungufu makubwa ambayo bila kuyabaini na ukaingia kichwakichwa, utakutana na matatizo makubwa.

Kwa maana hiyo basi, sifa hizi sita ambazo nitazizungumzia leo endapo utaziona kwa huyo ambaye macho yako yameganda kwake, fanya maamuzi sahihi ya kumkubalia.

Anakupenda kwa maana ya kukupenda
Unapoingia kwenye maisha ya ndoa, unatarajia kupata mapenzi ya kweli kutoka kwa mwenza wako. Wapo wanaume ambao wanaonesha wazi kutokuwa na mapenzi ya kweli bali wanakuwa na mapenzi ya kuzuga.

Wanachotaka wao aidha kupata umaarufu tu kwamba yuko na demu flani bomba au kuonja tu penzi kisha kuanza visa ili muachane.Kwa nini ni vizuri kumpata mwanaume mwenye mapenzi ya dhati? Hii inatokana na ukweli kwamba kinyume na hivyo, maisha yatakuwa ya migogoro kila siku. Atakufanyia mambo ya kukuumiza kwa kukusaliti bila kujali maumivu utakayopata. Hii yote ni kwa sababu hana mapenzi ya kweli na wewe.

Ndiyo maana unashauriwa kwamba, kabla hata ya kumuonjesha penzi kisha kufanya maamuzi ya kumruhusu aende kwa wazazi wako ili mfunge pingu za maisha, ni vyema ukawa na uthibitisho kwamba anakupenda kwa moyo mmoja.

Hili la tabia ndo’ kila kitu

Linapokuja suala la ndoa, tabia inakuwa kitu cha awali sana kuangaliwa. Hii ni kwa sababu, wapo wanaume ‘handsome’, wenye kazi nzuri na kipato kizuri lakini wanakosa sifa ya kuitwa mume kutokana na tabia zao chafu.

Hakuna mwanamke anayeweza kudiriki kumpa nafasi mwanaume kuwa mume wake wakati ana tabia chafu. Endapo utaangalia uzuri wa sura kisha ukafanya maamuzi ya kuolewa naye, utakuwa umejichimbia kaburi.

Awe anaota mafanikio
Hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko ya aina yake kwa wanawake. Wengi hawapendi kabisa kuolewa na mwanaume ambaye hana kazi.
Mwanaume anatakiwa kuwa dereva katika safari ya kusaka mafanikio, sasa kama atakuwa ni mtu wa kukaa kijiweni, kupiga mizinga, mvivu asiyependa kujishughulisha kwa namna yoyote, huyu hafai kupewa nafasi ya kuitwa mume.

Ile dhana ya kukubali kuolewa na mwanaume yoyote ili mradi upate heshima ya kwamba umeolewa, imepitwa na wakati. Mwanaume sahihi ni yule mwenye malengo maishani, anayefikiria nini cha kufanya kwa ajili ya maendeleo yake, mkewe na watoto wao.

Wa shida na raha
Wapo wanaume ambao siyo wavumilivu kabisa katika maisha.Tunajua maisha siku zote hayatabiriki, yanaweza kutokea matatizo ya kiafya ama kifedha.

Kwa mfano, unaweza kuingia kwenye maisha ya ndoa lakini kwa bahati mbaya ukawa huna kizazi, mwanaume mwenye mapenzi ya kweli na wewe anatakiwa kukuvumilia na kuwa upande wako.
Yule ambaye atakuwa anaungana na dada zake kukushambulia kwa kutozaa, hafai kuwa na wewe kwani yapo mengi yanayoweza kutokea yanayohitaji kuvumiliana.

Kimsingi uvumilivu kwa mwanaume utakuwepo kama tu atakuwa na mapenzi ya dhati kama nilivyozungumza hapo awali. Mwanaume mwenye mapenzi ya dhati ni lazima atakuwa mvumilivu na atakuwa tayari kuishi katika maisha ya aina yoyote, yawe ya raha ama ya starehe.

Anayejua thamani ya mke
Wapo wanaume ambao hawajui thamani ya mke na ukiwachunguza utabaini hawafai kuwa waume za watu. Mume sahihi ni yule anayejua kwamba mke ni kitu cha faraja kwenye maisha yake.
Yule anayeamini kwamba, bila mke maisha yake hayawezi kuwa yamekamilika. Wapo ambao wanaamini hata bila wanawake wanaweza kuwa na maisha mazuri.

Mwanaume mwenye dhana hii, ukimpa nafasi kwenye moyo wako na ukaingia naye kwenye maisha ya ndoa, lazima atakuwa mguu ndani, mguu nje. Hataona hatari kukupa talaka hata kwa jambo dogo tu ambalo mnaweza kuongea na mkalimaliza.

Ndiyo maana nikasema, mwanaume sahihi wa kumpa nafasi ya kuwa mumeo ni yule anayejua thamani ya mke, anayeweza kuvumilia yote akijua mke ndiye anayekamilisha maisha yake.

Asiye na tamaa za kijinga
Unaweza kuwa na mpenzi wa kawaida ukiwa na malengo ya kumfanya awe mumeo katika siku za baadaye. Huyu ukigundua ana tamaa, huna sababu ya ‘kumpetipeti’.
Wanaume wenye tamaa za kijinga ndiyo ambao wakishaingia kwenye maisha ya ndoa wanakuwa wepesi kusaliti. Hao hawastahili kuitwa waume za watu.

Mwisho kabisa naomba niseme kwamba, licha ya sifa hizo 6, yapo mambo mengine ambayo ukiyaona kwa mwanaume ambaye ulikuwa unahisi anafaa kuwa mumeo, ni vyema ukapingana na mawazo.
Mwanaume asiyepitwa na sketi, asiyependa kumsikiliza mwenza wake, anayependa kufanya maamuzi bila kutaka kumshirikisha mwenza wake, anayekuwa upande wa ndugu zake unapokuwa kwenye matatizo, asiyejali familia yake, anayekuona wewe si lolote, asiyethamini na kuwaheshimu ndugu na marafiki zako, huyo kaa naye mbali kabisa.

Ni hayo kwa leo.

GPL
Read More

Thursday, May 26, 2016

Saturday, May 7, 2016

Serikali Yabaini tani 4,579.2 za Sukari zilizokuwa zimefichwa


Taasisi ya kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU) imebaini kuwepo kwa sukari iliyofichwa  tani 4,579.2 iliyonunuliwa toka Kiwanda cha Sukari Kilombero.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Valentine Mlolowa Taasisi  hiyo imeanza uchunguzi dhidi ya swala hilo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa mnamo tarehe 05 Mei, 2016 timu ya uchunguzi ilitembelea maghala yaliyopo Tabata Jijini Dar es salaam na kubaini uwepo wa sukari hiyo.

TAKUKURU tayari imetembelea  Maghala ya mfanyabiasha Haruni Daudi Zacharia ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Al-Naeem yaliyoko Mbagala na Tabata ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa wa sukari hapa nchini na anayetuhumiwa kuficha bidhaa hiyo.

Aidha uchunguzi  uliofanywa na Taasisi hiyo ulibaini kuwepo kwa njama za dhati za kutouza  sukari iliyokutwa katika maghala hayo kulikofanywa na mfanyabiashara huyo kwani hata sehemu ya Maghala ilipo sukari hiyo hapakuwa na dalili za upakiaji wa sukari  hiyo ili iweze kusambazwa.

Taarifa hiyo imeendelea kufafanua kuwa katika eneo la Kitumbini  kumekuwa na wananchi wengi wanaohitaji  bidhaa hiyo na wachache sana waliweza kuuziwa  licha ya ukweli kwamba sukari ilikuwepo.

Katika uchunguzi wake TAKUKURU pia  imebaini kuwepo kwa mikakati ya dhati iliyokuwa ikifanywa na mfanyabiasha huyo kwa kununua sukari yote toka viwanda vya ndani na kisha kuihifadhi na kuuza bidhaa hiyo kidogo kidogo kwa wastani wa tani 250 kwa siku wakati alikuwa na uwezo wa kuuza zaidi jambo lililochangia uhaba wa sukari katika soko.

Kuficha bidhaa ni kosa la uhujumu uchumi na ni  kinyume na Aya ya 3 Jedwali la kwanza Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 [Chapisho la Mwaka 2002]. Serikali haitavumilia hujuma za namna hii na itachukua hatua kali dhidi ya mfanyabiashara yeyote ataekwenda kinyume na sheria hii.

TAKUKURU  inatoa wito kwa wafanyabiashara wote wa sukari kuacha vitendo vya kuficha sukari na vyombo vya uchunguzi vinafuatilia kote nchini na yeyote atakayebainika kufanya hujuma hizo atakabiliwa na mkondo wa Sheria.
Read More